DAVID KAFULILA APANGUA HOJA 7 ZA TUNDU LISSU KWA TAKWIMU



Na David KAFULILA,

Agosti 31, 2020.

Kwanza nashukuru sasa kuona ndugu yangu Tundu Lissu ameanza kuleta hoja zinazoweza kuanza kujadilika kama mgombea, tofauti na mwanzo ambapo ilikuwa ni masimulizi ambayo kwakweli hayakuwa na lolote la kusaidia maamuzi ya mpiga kura.

Jana nilifuatilia hotuba yake iliyokosoa masuala kadhaa ambayo nimeona si busara ayatumie kupotosha Watanzania kufanya maamuzi katika misingi ya upotoshaji.

Ili kurahisisha, nimepanga mawazo yangu katika mafungu 7;

1. Lissu anasema Ripoti ya Benki ya Dunia ya Mwaka huu 2020 kuhusu urahisi wa kufanya Biashara( Easy of Doing Business Report 2020) imeishusha Tanzania kutokana na utawala wa JPM.

Asichokijua Lissu na wenzake wanaotumia hoja hiyo ni kwamba tayari Benki hiyo hiyo ya dunia (WB), katika taarifa yake ya tarehe ya juzi Agosti 27,2020, imeifuta tathimini hiyo ya Mwaka 2020 na ile ya 2018.

 Benki ya Dunia imeleza wazi kuwa tathimini hizo zilikuwa na kasoro nyingi za kiuweledi na hivyo kukosa uhalisia. Kwa maelezo zaidi soma ....

Doing Business – Data Irregularities Statement

2. Lissu anashangaa inawezekanaje tuingie uchumi wa kati wakati tathimini ya taasisi ya MOODYS imeonesha Tanzania imeshuka daraja kutoka B1 Mwaka 2017 kwenda B2 Mwaka 2020 katika uwezo wa kukopa! ( credit rating).

Hili ni suala la uelewa tu kwani, kwanza; hakuna uhusiano kati ya madaraja ya uchumi yanayopangwa na Benki ya dunia na madaraja ya uwezo wa kukopa yanayopangwa na taasisi zinazofanya tathimini hizo (GLOBAL CREDIT RATING AGENCIES) ikiwemo MOODYS.

Ndio maana Mwaka 2017, Tanzania ilikuwa daraja la juu ( B1) kuliko Kenya (B2) kwenye ripoti za MOODY'S, ilhali Tanzania ilikuwa haijafuzu kuingia uchumi wa kati na Kenya ilikuwa tayari uchumi wa kati.

Kujua kwamba Tanzania ilipewa daraja la juu kuliko Kenya Mwaka 2017, soma Gazeti la Daily Business la Kenya la Machi4,2017-link

US agency assigns Tanzania higher credit rating than Kenya

Zaidi ni vema Lissu akafahamu kwamba kufuatia mtikisiko wa uchumi duniani uliosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa korona (COVID-19), nchi nyingi zimetikiswa kutokana na mtikisiko wa mnyororo wa biashara duniani (Global supply chain) ingawa ni kwa viwango tofauti.

Ndio maana hata Kenya ambayo Mwaka 2017, taasisi ya MOODYS waliwapa daraja la B2 ikiwa na alama chanya (B2 with positive outlook), Mwaka huu 2020, imendelea kuwa na B2 lakini kwa alama hasi (B2 with negative outlook).

Kiwango hicho ni chini ya Tanzania yenye daraja B2 chanya (B2 with positive outlook).

Sijui kwa mtazamo wa Lissu huenda Kenya iliyopewa na MOODYS daraja chini ya Tanzania Mwaka huu angesema nayo ishushwe daraja kiuchumi kiasi gani kutoka uchumi wa kati.

Pia ni vema ikafahamika kwamba serikali zinazoendeshwa kisasa duniani hutumia taasisi hizi kama MOODYS kufanyiwa tathimini. Na kwa Tanzania, kwa mara ya kwanza tumefanyiwa tahimini Mwaka 2017, chini ya JPM.

Hii ni kwasababu JPM anaamini katika usasa wa ukweli (real modernization) tofauti na Lissu anayedhani kuendesha uchumi kisasa ni kutozibana kampuni za madini kulipa kodi stahiki.

3. Hoja kwamba deni la Taifa wakati JK anaondoka lilikuwa trilioni 20 na kwamba katika awamu ya tano limeongezeka kufikia trilioni 40.

Hili nalo ni suala la ufahamu kwani ingawa kweli deni limeongezeka lakini takwimu hizo sio za kweli. Wakati Lissu anasema JK aliacha deni la Trilioni 20, ukweli ni kwamba deni la nje peke yake Mwaka 2015....lilikuwa zaidi ya dola Billioni 16.4 au zaidi ya Trilioni 30TZS wakati huo, achilia mbali deni la ndani ambalo lilikuwa zaidi ya Trilioni 8.7TZS. (Chanzo- BoT Monthly Economic review).

Usahihi wa takwimu na taarifa sahihi ni jambo muhimu sana hasa kwa Kiongozi anayetafuta kuaminika. Sijui Lissu hizi takwimu za trilioni 20 kazitoa vyanzo gani?

4. Lissu anasema uwezo wetu wa kuhimili deni umeshuka kwasababu deni limezidi kuwa kubwa.

Labda nitoe ufahamu wa jumla tu kwamba tatizo la deni kwenye uchumi wowote linapimwa kwa vigezo zaidi ya ukubwa wa deni, bali vigezo vya uhimilivu (debt sustainability).

Na dalili za wazi ambazo mtu wa kawaida anaweza kuzitumia kujua tuna tatizo la deni au lah!, ni kiwango cha riba unachotozwa kukopa.

Serikali inapokuwa na hali mbaya kiuchumi (desperate) inakopa kwa riba kubwa kuliko Serikali yenye hali nzuri kiuchumi.

Ndio sababu Mwaka 2015 kipindi ambacho serikali ilibidi kukopa ili kulipa mshahara watumishi, ilikopa soko la ndani kwa riba ya mpaka asilimia 17% kwa hatifungani za siku 365 Mwaka 2015, kulinganisha na kipindi cha JPM, ambapo Serikali inakopa kwa riba ya asilimia 4.8% kwa hatifungani za siku 365.

Hiyo ni hali ya kawaida hata kwa maisha binafsi, kwamba ukiwa hoi kiuchumi (desperate) hutojali ukubwa wa riba unapotaka mkopo, lakini ukiwa vizuri kiuchumi huwezi kuchukua mkopo kwa riba kandamizi.

Ninachojaribu kusisitiza ni kwamba afya yetu kiuchumi kumudu kukopa bado ni kubwa kwa vigezo vyote ndio maana Serikali inakopa kwa riba chini katika rekodi ya zaidi ya miaka10, na kwa vigezo vya tathimini za MOODY'S hakuna anayetuzidi afya hiyo ukanda huu.

5. Lissu anahoji umakini wa Serikali ya JPM kusimamia biashara na Sekta binafsi.

Kifupi JPM amerejesha biashara na sekta binafsi kwenye reli, kutoka biashara za mishentaun kwenda biashara halisi. Bahati mbaya kila nikiwasikiliza Lissu na Membe naona fikra zao ni turudi uchumi wa 'mishemishe'

Lissu anataka kupotosha Watanzania kama alivojaribu kwenye sekta ya madini wakati Rais alipoamua kuchukua hatua thabiti. Lissu alisema maamuzi ya madini yangeua sekta ya madini, lakini cha kushangaza mauzo ya dhahabu tu nje ( export) yameongezeka kutoka dola bilioni 1.3 mwaka 2015 mpaka dola bilioni 2.1 mwaka 2019.( BoT-MER)

Lissu anapotosha Watanzania kuwa biashara chini ya JPM tunafanya vibaya kuliko kabla, nimkumbushe tu kwamba namba hazidanganyi. Mauzo ya Tanzania nje ya nchi Mwaka 2015 yalikuwa dola bilioni 8.9 kulinganisha na dola bilioni 9.7Mwaka 2019.

6. Lissu anahoji uamuzi wa kununua ndege kwamba haukupitishwa na Bunge.

Labda hili lieleweke tu kwamba uamuzi wa kununua ndege haukupitishwa na upinzani bungeni sio bunge ingawa ilikuwa hoja ya upinzani mabunge yote kabla ya awamu ya tano kuingia na ilikuwa sehemu ya Ilani ya Chadema ya mwaka 2015 (rejea Ukurasa wa 40 Ilani ya Chadema).

Ukweli kauli ya Lissu kwamba Bunge halikuhusjshwa ununuzi wa ndege ni ya kusikitisha mno kutolewa na mgombea nafasi ya juu kabisa ya nchi.

Nasema hivi kwasababu bajeti ya ununuzi wa ndege kwa mara ya kwanza imepitishwa katika Bunge la Bajeti la 2016/17 ambapo ilitengwa na kupitishwa kiasi cha Trilioni 1.49TZS

Naomba ifike wakati ieleweke na tuweke kumbukumbu sawa kwamba tumetoka zama ambazo tulikodi ndege mbovu kwa dola milioni 43 mpaka zama za kununua ndege mpya bombardier kwa dola milioni 32...( Ripoti ya CAG , Aprili 2020).

Tumetoka zama za kujadili Taifa kukosa ndege mpaka zama za Taifa la kujadili namna ya kununua ndege (kwamba kununua kwa taslimu au kukopa). Huko nyuma hata uwezo wa kukopa hatukuwa nao.

7. Mwisho nihitimishe kwa kujadili hoja ya Lissu kuhusu Bima ya Afya nchini;

Labda niseme kwamba nilipokuwa Songwe kama Katibu Tawala Mkoa, wananchi vijijini walionesha mwitikio mkubwa sana kuhusu bima ya afya hata ile ya chini kwa maana ya CHF.

Songwe ulikuwa mkoa wa kwanza kwa kaya zenye bima ambapo asilimia76% walikuwa na bima hiyo.

Mwitikio wa wananchi kwa bima ni kitu halisi hasa baada ya Serikali kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. ( kutoka kutengewa billioni 31 mpaka billioni 270).

Ndio maana idadi ya Watanzania wanaotumia bima iliongezeka kutoka takribani wanufaika milioni 9.8 Mwaka 2015 mpaka zaidi ya milioni 16.7 mwaka 2019..

Nimshauri Ndugu yangu Lissu awe anafanya tafiti ya anayolishwa na wenzake kabla hajayamwaga majukwaani. Moja ya sifa za kiongozi bora ni kujiridhisha na taarifa kabla ya kuziweka hewani.

Mwisho.



Maoni

  1. asante sana. mh kafulila. ningeomba dalasa ili ungeliweka. fb. Twitter. ili wengi wajueukweli, 🙏

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

BE AWARE, Robert Amsterdam is a Canadian Set to Plant Violence in African Countries.

Ujumbe wa Wakili Msomi kwa Wanaharakati wa Kenya