CHADEMA Yalalamikiwa kupoteza Mvuto wa Kisiasa

''Mimi ni Mtanzania ninaishi nchini Marekani katika mji wa Chicago kiitikadi ni mfuasi wa CHADEMA, nimeguswa kuandika Makala hii kueleza masikitiko niliyonayo kwa vyama vya upinzani nchini hususani chama changu.

Nianze na kusema kuwa CHADEMA kilikuwa ni chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania hakikuwa na mpinzani kilijikita kuikosoa Serikali na kutoa mawazo mbadala, kwa sasa hali imekuwa ya tofauti kwani CHADEMA wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kukosoa na kutoa mawazo mbadala.

CHADEMA kwa sasa hawana agenda wamebakia kudandia agenda za Serikali na chama Tawala CCM, yani nimekuwa nikifuatilia hawana wanachokifanya wamebakia tu kulalamikia mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali bila kutoa ushauri wa nini kifanyike.

Naumia sana kuona chama changu kikishindwa kusimama katika nafasi yake, mpaka vyama vya wasaliti vilivyoanza juzi tu vinaanza kuleta upinzani. Najiuliza tatizo nini? Je ni mfumo wa uongozi? Je viongozi kutojua majukumu yao? 

Hivi karibuni nimeshuhudia wanachadema wezangu hasa vijana wakifanya harambee za kuchangisha fedha wakidai kuwa fedha hizo watazitumia kulipa faini watuhumiwa wa makosa mbalimbali ambao ni wanachama wetu, hii si sawa kwa sababu wanachofanya ni ubaguzi kwa Watanzania kama nia yao ni kusaidia basi walipaswa kutoa msaada bila kujali chama ili kukitangaza chama.

Kwa upande wa Bawacha wao ndo wamenishangaza kufanya press conference, kuandaa maandamano ya kutaka wanawake wezao ambao wanawawakilisha Bungeni waondolewe? Najiuliza je hayo ndio majukumu pekee waliyonayo? Nilitegemea wao wawe namba moja kutetea haki za wanawake nchini na ndani ya Chama lakini wamegubikwa na mfumo dume mpaka wamesahau haki zao za msingi.

Bawacha walipaswa kuwa msitari wa mbele kupigania haki za wanawake tena kwa wakati huu hii ni nafasi yao kwani mkuu wa nchi ni mwanamke walipaswa kumshauri Mhe. Rais ili atatue changamoto wanazokumbana nazo.

Sakata la wabunge 19 wa viti maalum binafsi naona Chama chetu kimeweka jambo hilo kwenye mtego wa kutaka kurumbana na serikali wakati wao ndo suluhu ya jambo hilo kwa sababu wabunge hao walifukuzwa chama lakini wakakata rufaa mpaka leo chama hakijawajibu rufaa kwa nini? 

Nakumbuka kipindi cha Sakata la Zitto kuitwa msaliti chama kilijibu rufaa mapema na Zitto akafungua kesi mahakamani mwisho wa siku sintofahamu ikatatuliwa na Mahakama, hicho ndo kinachowafanya viongozi kuhofia kujibu rufaa za wale wabunge 19. Kwa sababu wale wabunge wakiongozwa na Halima Mdee wamejiandaa vya kutosha siku wakijibiwa tu rufaa wanaenda kufungua kesi ya madai ya kuonewa ndani ya Chama.

Hivyo viongozi wanajua na wanaelewa kuwa kwenye hiyo kesi hawawezi kuchomoka ndio maana wanaendelea kujivuta huku wakisuguana na Spika wa Bunge ili siku ziendelee kusonga mbele. Bavicha kwa sasa naona wamepewa agenda hii ya kumshambulia Spika ili kufanya mgogoro uwe mkubwa na kumkasirisha Spika ili aamue kuwafukiuza wabunge hao Bungeni.

Haya ni mapungufu machache niliyoyabaini kuhusu Chama changu, na nayaona ni hatari kwa sababu yanasababisha chama chetu kupoteza mvuto wa kisiasa. Natoa wito kwa viongozi wa chama kurudi nyuma kujitathimini, pamoja na kujikita katika agenda za chama kushauri Serikali kwa kutoa njia mbadala ya kutekeleza mambo mbalimbali ya kimaendeleo badala ya kupinga kila kitu kinachofanywa.

Tuache siasa za kushambuliana Tujenge Nchi yetu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kabla ya kumyoshea mwingine kidole.''

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Manufaa ya Ushirikiano wa Tanzania na Kenya

BE AWARE, Robert Amsterdam is a Canadian Set to Plant Violence in African Countries.

LICHA YA AHADI KUWA WANGESHIRIKIANA, LISSU NA MEMBE KILA MMOJA ANAGOMBEA “KIVYAKE.”